NAOMBA

furaha2

(photo by amkatanzania.com)

 

Nimechoka Uchovu Wangu Ni Mchoko Wa Moyo.

Nimechoka Mateso Yanadhihaki Utayari Kumoyo.

Sina Hadhi Wandani Wameniuza Kwa Choyo.

Masimango Ninakula Kokoto Kibogoyo.

Nina Hamu Kurudi Nyumbani Ila Bado Sipaoni.

Kwa mbali Roho Inatamani Macho Yangu Yamekosa Harubini Hata Miwani.

Siku Hizi Najicheka Kwa Kebehi,

Nakitazama Kioo Sura Yangu Haitokei.

Natamani Sana Kurudi Nyuma, Mbele Milima Imeniziba Sioni.

Safari Bado Ni Changa, Machozi Yamekuwa Makovu Mbele Kusonga Maumivu.

Nakumbushwa Yamenikuta Nilipohasi Tulivu.

Nasikia Nimekosa Usikivu.

Ndizi Mbichi Nazichoma Nimekosa Zile Mbivu.

Nataka Kupendwa-penda Mpendwa, Upendo Majani Makavu.

Nimlaumu Nani Yakinipiga, Yakinizonga, Yakinibana Mbavu.

Nawalaumu, Nawalaumu, Ila Siwalaani.

Nimewahukumu Kwa Msamaha Mara Saba Sabini,

Hawajasema Samahani.

Nimesahau Japo Kiukweli Ninaishi Na Zamani.

Ninaketi Na Maswali Ya Kwanini Yananiangalia Tu Sijui Kiburi Au Ndo Gawio La Yangu Sahani.

Huku Nilipo Sina Amani. Moyo Unaugua Sina Raha Jamani.

Na Haya Nawaandikia Nikiwa Utumwani.

Bado Lile Pendo La Zamani Lanifariji Mwanenu.

Nikilikumbuka Nalikumbata Linijaze Furahani.

Mengi Makwazo, Yangu Mawazo, Yananitoa Rahani.

Kwanini Niyapitie Haya? Eeh Mungu Nipinguzie, Nifutie Hili Chozi Moyoni.

Yapo Uliyofuta Nafurahi Ndio Maana Nakuja Kukuomba Tena Baba Nipokee Ombi Langu Rohoni.

Fabian M. Christophe
Babananiii©2016

Leave a comment